Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan, katika tamko lake amelaani vikali mpango wa utawala wa Kizayuni wa kuikalia Ghaza na kulieleza tendo hilo kuwa ni kofi kali usoni mwa jamii ya kimataifa, aidha amesisitiza kuwa, baada ya jinai hizi za kutisha, kutumia jina la “dunia yenye ustaarabu” kwa ajili ya madola ya kimataifa ni matusi ya dhahiri kwa maana halisi ya ustaarabu.
Rais wa Baraza la Maulamaa wa Kishia Pakistan ameendelea kueleza kuwa; hali ya Ghaza leo imefikia hatua ya maafa makubwa sana; ambapo katika ardhi hii ndogo iliyozingirwa, watu wasio na ulinzi wanakabiliana na njaa, uharibifu, kukosa makazi na vifo vya halaiki, wakati maafa haya yote yakitokea, mataifa duniani, aidha yanacheza nafasi ya kuwa waungaji mkono wa moja kwa moja wa dhulma, au yamo katika kimya cha mauti, yakitazama jinai hizi. Kiwango hiki kikubwa cha ukatili na unyama hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya karibuni, na katu hakitasahaulika katika kumbukumbu za mataifa.
Aidha, huku akipinga vikali misimamo dhaifu ya nchi mbalimbali, amesema kuwa matamko ya kulaani na ya kuonyesha wasiwasi – iwe kutoka kwa jamii ya kimataifa au hata kutoka Pakistan – hayatapunguza lolote katika maumivu ya watu wa Ghaza waliodhulumiwa, msimamo wa aina hii ni sawa na kufumbia macho dhulma iliyo wazi na kuendeleza maafa haya.
Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Kipakistani, akirejelea nafasi maalumu ya Pakistan katika ulimwengu wa Kiislamu na umuhimu wa uwezo wa nyuklia wa nchi hii, amekumbusha kuwa sifa hizi zinabeba jukumu zito la kihistoria na la kisheria juu ya mabega ya Pakistan.
Ameendelea kukumbusha kuwa; Pakistan tangu kuasisiwa kwake, imekuwa na uhusiano wa karibu na suala la Palestina, na kwamba leo ina wajibu wa kuchukua hatua zinazozidi misimamo ya maneno matupu. Pakistan inapaswa kutumia uwezo wake wote wa kisiasa na kidiplomasia kusimama pamoja na taifa la Palestina lenye kudhulumiwa na kutoa msaada wa kivitendo kwao.
Mwanazuoni huyu mashuhuri wa Kipakistani, katika kuhitimisha kwake, ametoa onyo kwamba wakati wa kauli za maneno umekwisha, na leo ni siku ambayo mataifa na serikali zitapimwa na historia kwa matendo yao halisi. Amesisitiza kuwa; Pakistan inapaswa kuwa mstari wa mbele katika safu ya wanaounga mkono Palestina, na kwa vitendo dhahiri ithibitishe uaminifu wake kwa haki na utetezi wa wanyonge duniani.
Maoni yako